SIKU 10 ZA MAOMBI | JANUARI 7-17, 2026

Karibu katika KUFUNGULIWA! Tunaamini kwamba Yesu Anakuja hivi karibuni. Hivyo, mada kuu ya Siku 10 za Maombi mwaka huu ni
kumwalika Roho Mtakatifu abadilishe maisha yetu na ulimwengu wetu. Jiunge nasi tunapomtafuta Mungu kwa siku 10 za uamsho tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
Kabla hajafa, Yesu aliwaahidi wafuasi Wake zawadi ya Roho Mtakatifu: “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli” (Yohana 14:16, 17). Baadaye, mara kabla hajaondoka duniani na kwenda kuandaa mahali pa milele kwa ajili yetu, Yesu aliwaagiza wanafunzi Wake wasitoke Yerusalemu “bali waingoje Ahadi ya Baba,” ambayo ni ubatizo wa Roho Mtakatifu (Mdo. 1:4, 5).
Hata hivyo, zawadi hii iliyoahidiwa kwa kiasi kikubwa haijafunguliwa na watu wa Mungu. Huwa tunaizungumzia tu Zawadi hii. Tunajifunza na kuichunguza Ahadi hii. Lakini mara nyingi hatufikii hatua ya kuifungua Zawadi hii ya Roho Mtakatifu.
Bila ya shaka, ni Roho Mtakatifu pekee anayeweza kuifanya upya mioyo yetu yenye dhambi: “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ezekieli 36:26).
Ni Roho Mtakatifu pekee anayeweza kubadilisha watoto wetu: “Nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu ya yao utakaowazaa” (Isaya 44:3).
Pia ni Roho Mtakatifu tu anayetuunganisha na familia ya Mungu mbinguni: “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:16).

Lililo bora zaidi, Mungu yuko tayari kutupatia Roho Mtakatifu: “Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” (Luka 11:13).
Ahadi ipo tayari, ikitusubiri tuidai. Ellen White anaandika, “Kama wote wangekuwa na nia hiyo, wote wangejazwa kwa Roho. Popote ambapo hitaji la Roho Mtakatifu, linachukuliwa kuwa jambo lenye uzito mdogo, kumeonekana kuwa na ukame na giza la kiroho, kushuka kwa hali ya kiroho na kifo.” Anauliza pia, “Kwa kuwa hii ndiyo njia pekee tunayoweza kupokelea nguvu, kwa nini hatuhisi njaa na kiu ya karama ya Roho? Kwa nini hatuzungumzii, wala kuomba ama kuhubiri habari za Roho Mtakatifu?” (Matendo ya Mitume, Sehemu ya Kwanza, uk. 40).
Roho Mtakatifu aliye ndani yetu anatujaza upendo wa Baba na kutuwezesha kuwa mashahidi wasio na hofu na wa kufaa kwa ajili ya Kristo. Kwa nini usiombe kwa ajili ya Zawadi hii?

Tazama Ardhi Ikitetemeka
Katika 1 Samweli 14 tunapata kisa cha kusisimua cha Yonathani na mbeba silaha wake. Wakati baba yake, Mfalme Sauli, alipokuwa chini ya mkomamanga akiwa hafanyi chochote, Yonathani na mbeba silaha wake walitoroka kutoka katika eneo lao salama kuelekea katika utukufu wa Mungu. Jeshi la Wafilisti lilikuwa likiitisha Israeli; sasa jeshi lao kubwa lilikuwa limepiga kambi ng’ambo ya korongo refu, likisubiri kupigana na Israeli.
Wakisukumwa na imani yao kwa Mungu, Yonathani na mbeba silaha wake walisombera wakishuka kwenda chini korongoni na kisha wakapanda juu ya miinuko ng’ambo

ya pili ili kukabiliana na jeshi la adui peke yao. Bila hofu, mashujaa hawa wawili, walikabiliana na Wafilisti kwa nguvu za Bwana. Walipigana na kikosi kizima cha askari Mungu mwenyewe akiingilia kati. Biblia inasema “tetemeko la Mungu” lilitetemesha kambi, shamba na watu wote [1 Samweli 14:15, (Tafsiri Sisisi ya Young)]. Imani ya Yonathani ndiyo iliyompa Mungu sababu ya kufanya ardhi itetemeke mbele ya hawa mashujaa wawili. Kama Mungu asingeingilia kati kwa kutoa tetemeko la ardhi, Yonathani na mbeba silaha wake wangeshindwa kirahisi.
Mungu bado anatenda duniani leo. Jiunge nasi tunapoomba, “Ee Mungu, ni nini kitakachokupa sababu, siku 10 mfululizo, kufanya ardhi itetemeke?”
Miaka elfu mbili iliyopita, takribani waumini 120 walikusanyika kwenye chumba cha ghorofa ya pili ya nyumba juu ya mitaa iliyosongamana ya Yerusalemu. Walithubutu kuamini ahadi ya Yesu ya Roho Mtakatifu. Walithubutu kuitii amri ya Yesu ya kuingojea Zawadi hii (Mdo. 1, 2).
Hivyo walikusanyika, wakasubiri. Roho Mtakatifu alipomiminwa wakati wa Pentekoste, waumini walifunguliwa kuwa mashahidi hai wa Mwokozi aliyefufuka, Yesu Kristo! Walizipenda familia zao na familia ya imani kuliko wakati wowote uliopita. Walitoa kwa kujitolea zaidi ya walivyofanya hapo kabla. Walisimama na kuthubutu kusema habari za Kristo kuliko wakati wowote hapo kabla.
Roho Mtakatifu anapenda kufanya kazi kutoka ndani kwenda nje! Tunakukaribisha upate uzoefu wa Siku 10 za Maombi si kama utaratibu tu, bali kama mtindo mpya wa maisha.

KUFUNGULIWA! ina sehemu tatu kila siku:
Wakati wa Pekee Pamoja na Mungu
Kila siku ya siku 10 za maombi; anza kwa maombi binafsi na kusoma Biblia.
 
Wanafamilia/Marafiki
Tumia muda kukusanya familia yako au mzunguko wa marafiki kwa ajili ya maombi ya kila siku.
 
Familia ya Kanisa
Jiunge na familia yako ya kanisa kwa ajili ya kipindi cha maombi yenye vizazi tofauti kila siku.
 
Kusanya marafiki, washiriki wa kanisa, wafanyakazi wenzako, vijana na watoto wa rika zote kwa siku 10 za uamsho wa kiroho. Ni wakati wa kufunguliwa kikamilifu na Roho Mtakatifu tena!

Mwongozo wa Kiongozi – KUFUNGULIWA!
Kila siku ya siku 10 za Maombi itajumuisha sehemu tatu:
Wakati wa Pekee Pamoja na Mungu (Ibada Binafsi)
Furahia sehemu hii kila siku, wakati wa peke yako pamoja na Mungu. Kila mtoto anayeweza kusoma, kila kijana na kila mtu mzima anaalikwa kukutana na Mungu katika Neno lililoandikwa, kuomba na kutembea pamoja na Yesu.
Wanafamilia/Marafiki (Ibada ya Familia)
Alika familia yako au rafiki zako kutumia muda pamoja na wewe. Yeyote unayemhesabu kama mwanafamilia na awe sehemu ya muda huu. Waombee kwanza, kisha wakusanye kwa ajili ya wakati huu wa thamani katika Neno la Mungu na maombi.
Familia ya Kanisa (Mkusanyiko wa Kila Jioni) Karibisha kanisa lako, majirani na jumuiya ya marafiki kukusanyika mara moja kila siku kwa ajili ya maombi haya na shughuli hizi. Omba kwa dhati ili Mungu akuoneshe nani umwalike ili kuongeza washiriki walio hai kanisani kwako. Tafakari kwa maombi namna ya kuwaalika wewe binafsi washiriki wasio hai, washiriki wa zamani, wale uliosoma nao, wafanyakazi wenza na viongozi wa kidini wa madhehebu mengine.
 
Kanuni za Kufanya katika Siku 10 za Maombi Ziwe kwa Ajili ya Vizazi Changamano
Kikundi chetu cha maombi watakutana na kupanga maombi ya watu wawili ili kuomba kwa ajili ya kila mtoto, kijana na mtu mzima kwa kumtaja kwa jina kila siku. Ikiwezekana tutawaombea kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza siku 10 za maombi. Tutatoa

nafasi kwa watu wawili wawili kuomba kwa ajili ya watu 10 kwa kutaja majina yao kabla na wakati wa siku 10 za maombi. Tutaomba kwamba Roho Mtakatifu aandae kila moyo kulipokea Neno la Mungu lililoandikwa na kufunguliwa Naye.
Tutatumia Neno la Mungu lililoandikwa kama mwongozo wetu wa msingi. Tutafanya kila linalowezekana kwa ajili ya upatikanaji wa Biblia kwa watu wazima wote na watoto wanaoweza kusoma. Pia kila siku tutabarikiwa kwa maneno yenye kuleta msukumo kutoka kwa Ellen G. White.
Wale tunaojitolea kualika familia ya Kanisa ili kuomba, tutajitolea kwanza katika:
Kutenga kila siku wakati wa pekee pamoja na Mungu katika maombi na Neno Lake.
Kujisalimisha kwa Yesu kama Bwana
Kuomba na kupokea kwa imani ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Tutajumuisha kila rika katika vikundi vidogo vyenye watu sita au pungufu ya hapo vikiongozwa na mwanafunzi mmoja na mtu mzima mmoja kwa ajili ya kila mkutano wa familia ya Kanisa.
Tutachagua hawa viongozi wa vikundi hivi vidogo (wawili kwa kila kikundi: mtu mzima mmoja na mtoto/kijana mmoja) kwa maombi ya dhati na kumngojea Mungu na kuwaandaa viongozi hawa kuongoza watu wao kama wanaowafanya kuwa wanafunzi.
Tutajumuisha rika zote kadiri inavyowezekana katika kila sehemu ya kuongoza Maombi haya ya Siku 10 na tutajitahidi kufanya kila sehemu ieleweke kwa mtoto mwenye umri wa miaka 10.

Tutafanya maombi yetu kuwa mafupi ili kila mtu katika kikundi chetu aweze kushiriki. Mara nyingi, ombi la sentensi moja au mbili linatosha na kufanya wakati huu uwe wenye kuvutia kwa ajili ya watoto na vijana.
Tutajitahidi kuongoza kila mtu katika kushiriki kwa vitendo katika Siku 10 za Maombi, kuliko kuwa mtazamaji.
Tutaimba nyimbo zenye kuleta tafakari kwa rika zote na kusaidia kila mtoto, kijana na mtu mzima kujua kuwa wanayo sauti katika ibada.
Tutasalimisha mipango yetu ya kila mkutano kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.
Tutatoa chakula chepesi cha jioni kabla ya kila mkutano wa familia ya Kanisa ili kuutia moyo ushirika wa waumini kama ilivyo katika kitabu cha Matendo ya Mitume (taz. Mdo. 2:42).
 
Namna ya Kuongoza Siku 10 za Maombi kwa Ajili ya Matokeo Makubwa
Siku kumi kabla ya Siku 10 za Maombi kuanza: Soma na kuomba katika sehemu zote za mwongozo wa kila siku: Wakati Pekee Pamoja na Mungu, Wanafamilia/ Marafiki na Familia ya Kanisa.
Wakati wa Siku 10 za Maombi: Soma na kuombea mwongozo wa kila siku tena. Tunatumaini, wewe binafsi utapitia uzoefu wa nguvu ya Neno la Mungu likiambatana na Roho Mtakatifu kabla ya kulialika kanisa lako kufanya vivyo hivyo.
Hakikisha Muda Pekee Pamoja na Mungu na Familia/Rafiki unapatikana kila siku kwa kila mtu anayehudhuria kipindi cha jioni cha Familia ya Kanisa.

Kwa ajili ya Familia ya Kanisa kila siku:
Omba pamoja na viongozi wote wa vikundi vidogo, viongozi wa maombi na viongozi wa nyimbo dakika 30 kabla ya kipindi kuanza.
Elekeza vikundi vidogo vyote kutoka mbele kwa
ajili ya maombi na maelekezo kutoka kwenye Neno ili vikundi hivyo vianzishwe na viunganishwe katika maombi na kujifunza Neno.
Jipatie changamoto ya Saa 24 wewe mwenyewe
ya kufuata mambo haya kila siku ili uwe mkweli unapouliza kila mtu alifanya nini katika changamoto hiyo siku inayofuata.
Kwa maombi mengi, shiriki wito pendekezwa
kutoka moyoni mwako. Usiusome. Omba na wale wanaoitikia na wale wasioitikia.
Jiandae kushiriki ushuhuda wako mwenyewe
kuhusu jinsi kifungu cha Maandiko cha kila kipindi kinavyoathiri maisha yako. Toa ushuhuda wako kabla ya wito—ukionesha nguvu ya Kristo ya kubadilisha maisha kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, si kwa nguvu zako binafsi.
Funga mkutano kwa kumshukuru kila mtu kwa
kuwa sehemu ya kile ambacho Mungu anafanya katika Siku 10 za Maombi.
Baada ya kila mkutano, jitayarishe kwa miadi ya
Kiungu na wale wenye maswali au wanaohitaji maombi.
Panga Mkutano wa “Kipi Kinafuata?” utakaofanyika mara moja baada ya Siku 10 za Maombi. Hizi siku 10 za maombi si mwisho kwa zenyewe. Roho Mtakatifu yupo tayari zaidi kufanya mikutano hii iwe kichocheo cha utume binafsi, wa kifamilia na wa familia ya kanisa katika jamii yako na ulimwenguni

kote! (Angalia muhtasari uliowekwa kwa ajili ya Mkutano wa “Kipi Kinafuata?”)
Vitu Unavyohitaji kwa Ajili ya Mikutano ya Jioni ya Familia ya Kanisa:
Eneo la mkutano lililo kubwa la kuwatosha
washiriki wote kukaa katika vikundi vidogo vya watu sita.
Kiongozi    wa     maombi mwenye      kukubali
mabadiliko kuongoza vipindi vya Familia ya Kanisa kutokea mbele.
Wajumbe wa ziada wa timu ya maombi kupanga
na kuandaa nyimbo za wakati wa maombi ya vikundi.
Viongozi wawili (mtu mzima mmoja na kijana
mmoja) kwa kila kundi dogo lenye watu sita.
Biblia kwa washiriki wote (wanaweza kuleta za kwao au mnaweza kuwapatia).
Nakala za mwongozo wa kila siku wa maombi
kwa   washiriki   (au   ufikishwe         kidigitali    ikiwa inapendelewa).
Kwa ajili ya Mkutano wa Kipi Kinafuata?: ubao
mkubwa wa kuandikia na kuweza kufuta, kalamu maalumu, karatasi zenye gundi au karatasi/utepe.

Mtiririko Unaopendekezwa kwa Ajili ya Mikutano ya Jioni ya Familia ya Kanisa (pamoja na muda unaopendekezwa)
 
6:00 Chakula chepesi cha jioni
6:30 Maombi na viongozi wote wa vikundi vidogo, viongozi wa maombi na viongozi wa nyimbo
7:00 Ukaribisho (kutoka mbele kwanza kisha katika vikundi vidogo)
7:03    Ibada katika Maombi
Shukrani/Sifa (mojawapo)
Ungama/Tubu (mojawapo)
Omba
7:25 Shuhudia(shirikiana katika vikundi vyenu kile Mungu alichokusaidia kufanya katika Changamoto ya Saa 24)
7:30 Shughuli ya Kushirikiana
7:35    Ibada katika Neno (Maandiko na majadiliano) 7:45         Kusudi la Maombi
7:55    Wito/Maombi/Kushiriki Changamoto ya Saa 24 8:00                 Washukuru watu kwa kuja na wape ruhusa ya
kuondoka
 
Machapisho ya Siku Kumi za Maombi yameandaliwa na Chama cha Wachungaji, Konferensi Kuu ya Waadventista wa Sabato. Copyright © 2025. Mchangiaji Mkuu: Don MacLafferty.

Mkutano wa Mwisho: “Kipi Kinafuata?”
Vitu Vinavyohitajika, Ikiwa Vinapatikana:
Ubao mkubwa unaoweza kufutika (dry erase board) au kitu cha kufanana, kinachoweza kugawanywa katika sehemu 4, AU mbao 4 ndogo zilizowekwa kwenye viweko.
Karatasi zenye gundi (Sticky notes, ikiwa zinapatikana) AU vipande vidogo vya karatasi na utepe vya kushikiza kwenye ubao.
Kalamu maalumu zinazoweza kufutika (Markers za dry erase) kwa ajili ya kuandikia vichwa vya kila sehemu AU karatasi, kalamu na utepe ikiwa unataka kushikiza vichwa ili kuviweka mahali pengine.
 
Kwa Nini?
Roho Mtakatifu amekuwa akitenda kazi katika maisha yako na kanisa lako! Fuatilia mara moja Siku 10 za Maombi kwa kuwakusanya watu wa Mungu pamoja ili kuomba na kutafuta mpango Wake. Hatari inaweza kuwa kurudi kwenye taratibu za zamani na kupoteza msukumo aliouunda Mungu katika siku hizi za maombi yanayobadilisha maisha. Panga kukutana pamoja haraka iwezekanavyo!
 
Ni Kitu Gani?
Mkutano huu ni kwa ajili ya kutafuta kile Mungu anachotuita kukifanya katika maeneo manne:
Eneo binafsi
Eneo la wana Familia/Marafiki
Familia ya Kanisa
Eneo la jamii pana/Ulimwengu

Kwa Namna Gani?
Hapa kuna pendekezo moja la namna ya kuendesha mkutano. Mwombe na kumsihi Mungu akusaidie kuongeza au kupunguza chochote katika muhtasari huu kulingana na kanisa lako.
 
Muhtasari wa Kipindi cha Mwisho
Mkutano unapoanza, ketisha familia au wanandoa pamoja. Waombe wengine waunde vikundi vidogo ya marafiki, ikihakikishwa kila mtu anashirikishwa. Uwe na viongozi walio tayari kusaidia kujumuisha kila mtu katika kikundi.
Ukaribisho na Maombi Shughuli ya Kushirikiana
KIONGOZI KWA WOTE: Jadili maswali yafuatayo na kundi la familia/marafiki:
Taja tukio moja maishani ambalo ulijisikia kuwa umejiandaa kwalo zaidi.
Kisha, taja tukio moja maishani ambalo ulijisikia kutojiandaa vya kutosha kwalo.
Kumwabudu Mungu kwa Shukrani (WOTE)
Imba wimbo wa shukrani na kundi lote.
Waalike wanaojitolea kushiriki kile Yesu Kristo alichofanya katika maisha yao wakati wa Siku 10 za Maombi.
Imba wimbo mwingine wa shukrani pamoja.
Mtu mmoja aombe kwa ajili ya ujio wa Roho Mtakatifu ili kuongoza mkutano huu.
Mtu mmoja asome Waefeso 3:20, 21 kwa kundi lote. Aya hii inapaswa kuathiri vipi kanisa tunapojitayarisha kwa kile kinachofuata? Waalike washiriki kushiriki mawazo yao.

Weka ubao mkubwa ulio na sehemu 4, (au uweke mbao 4 ndogo mbele ya kila mtu ili aone). Tambua sehemu nne: BINAFSI, FAMILIA/MARAFIKI, FAMILIA YA KANISA, JAMII/ULIMWENGU.
 
KIONGOZI KWA WOTE: Tunamwomba Mungu atuoneshe hatua maalumu za kuchukua katika maeneo haya manne. Si mawazo ya jumla, bali yale yaliyo mahususi na yanayoweza kupimika. (Mfano: SI “Kuwa vizuri zaidi kiroho,” bali,“ kuwa na wakati wa pekee usioingiliwa wa kuwa pamoja na Mungu katika Neno Lake na maombi KABLA ya kifungua kinywa kila siku.”)
 
Binafsi
Mpatie kila mtu karatasi za gundi na kalamu. Jumuisha rika zote.
Waalike watu wote kuwa na muda wa kuomba kimya. Mwombe Mungu kwa kitu kimoja ambacho anakuita kufanya kama hatua binafsi katika uamsho wako pamoja na Yesu.
Andika kwa ufupi kwenye karatasi sentensi moja au neno moja. Waalike washiriki kugundisha karatasi kwenye sehemu ya “Binafsi.” (Pia wanaweza kuzitunza.)

Wanafamilia/Marafiki
Toa karatasi moja yenye gundi kwa kila kundi la familia/marafiki.
Waalike kuomba pamoja. Wamwombe Mungu kitu kimoja ambacho kitasaidia familia au kanisa kukua na kupata mwamko wa kila siku.
Jadili.
Andika kwa ufupi na bandika kwenye sehemu ya “Familia / Marafiki.”
 
Familia ya Kanisa
Waombe washiriki wagawanyike na kuunda vikundi vidogo vidogo vyenye watu 6 au pungufu katika Siku 10 za Maombi. (Ikiwa washiriki wapya hawapo katika kundi lolote, wagawe kuwa sehemu ya vikundi vilivyopo.)
Alika vikundi vidogo kuomba pamoja. Wamwombe Mungu kitu kimoja ambacho kitaisaidia familia ya kanisa kupata uzoefu wa uamsho wa kila siku pamoja na Yesu.
Jadili.
Andika “kitu kimoja” na bandika kwenye sehemu ya “Familia ya Kanisa.”

Jamii/Ulimwengu
Toa karatasi nyingine yenye gundi kwa kila kundi dogo.
Waalike kuomba. Wamwombe Mungu awafundishe njia moja ya kuifikia jamii na ulimwengu kwa habari njema ya Yesu. Fikiria kitu cha wakati huu na kinachohusiana.
Jadili.
Andika “kitu kimoja” kwa sentensi moja na bandika kwenye sehemu ya “Jamii/Ulimwengu.”
 
(WOTE)
Tengeneza mduara na mwombe Mungu azibariki hatua hizi zinazofuata.
Waambie washiriki wa Siku 10 za Maombi kwamba wachungaji au wazee wa kanisa watachunguza maoni haya, kuyaombea na kutoa mapendekezo katika baraza la kanisa na washiriki kuhusu hatua zinazofuata ambazo kwa pamoja na Kanisa mnaweza kuzipiga. Kwa pamoja jitahidini kuishi maisha mapya ya maombi. Hebu mtazame Roho wa Mungu anapokuwa akifunguliwa kwa nguvu nyumbani kwako na kanisani kwako!

+ Show More
– Show Less

Mjue Yesu kama Mwokozi Wetu Aliye Hai

Matendo ya Mitume 1:1-3
Wakati wa Pekee Pamoja na Mung
Ombi
Dai Zaburi 119:105 katika maombi. Mwombe Mungu akutumie Roho Mtakatifu kulifanya Neno lililoandikwa kuwa taa katika safari yako ya imani.
Chunguza Neno
Soma Matendo ya Mitume 1:1-3. Je, kifungu hiki kinakufundisha nini kuhusu Yesu?
Chunguza vitabu vinne vya Injili ili kuona ni mara ngapi Yesu amejidhihirisha Mwenyewe kuwa YU HAI kwa wanafunzi Wake baada ya ufufuo Wake. (Tazama Mt. 28:9-20; Marko 16:9-20; Luka 24:13- 53; Yohana 20:14 hadi 21:25.)
 

Hekima kutoka kwa Ellen White:
Kwa muda wa siku arobaini, Kristo alibaki duniani, akiwaandaa wanafunzi Wake kwa kazi iliyokuwa mbele yao na kuendelea kuwafafanulia kile walichokuwa wameshindwa kukielewa hadi wakati huo. Alizungumzia unabii wa kuja Kwake, kukataliwa Kwake na Wayahudi, pia kifo Chake, akionesha kuwa kila hatua ya unabii huu ilikuwa imetimia. Aliwaambia kwamba kutimia kwa unabii huu ilipasa wauchukulie kama uthibitisho wa uwezo watakaokuwa nao kwenye kazi iliyo mbele yao. Nasi tunasoma, “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote yatahubiriwa kwa jina

Lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.” Akaongezea, “nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.”
Siku zile Yesu alizozitumia na wanafunzi Wake, walipata uzoefu mpya. Walipokuwa wakimsikiliza Bwana wao akiyafafanua Maandiko Matakatifu katika nuru ya kile kilichokuwa kimetokea, imani yao Kwake iliimarishwa kikamilifu. Walifika hatua ya kuweza kusema, “namjua yeye niliyemwamini.” 2 Timotheo 1:12. Tangu hapo walianza kuona aina na ukubwa wa kazi waliyokuwa nayo, na kuona kwamba walikuwa waende kuutangaza ukweli waliokuwa nao kwa ulimwengu. Matukio ya maisha, kifo na ufufuo wa Kristo, unabii uliokuwa unaelekeza kwa matukio haya, mafumbo ya mpango wa wokovu, uweza wa Yesu wa kuondoa dhambi – wao walikuwa mashahidi wa mambo yote haya, na walikuwa waende wakayatangaze kwa ulimwengu. Ilikuwa inapasa kuitangaza Injili ya amani na wokovu kupitia toba ya dhambi na uweza wa Mwokozi. (Matendo ya Mitume, Sehemu ya Kwanza, uk. 20)
Kusudi la Maombi
Tumia muda mfupi kufikiria juu ya maisha yako. Mwambie Mungu baadhi ya njia ambazo Bwana Yesu amekuonesha kwamba Yeye yu hai! Mshukuru Mungu kwamba Yesu Kristo amejidhihirisha Mwenyewe kupitia kwa majibu ya maombi kama Mwokozi aliye hai.
Wanafamilia/Marafiki
Shughuli ya Kushirikiana
Mwalike rafiki au mwanafamilia ili aweze kuelezea kwa ufupi kitu bila kukitaja kwa jina lake hasa. Toa sababu moja kwa nini unajua kuwa kitu hicho kipo hai. Kila mtu

ajaribu kubaini kile unachokielezea. (Kwa mfano: Anayo mabawa na anavutiwa na uzuri wa shamba. Ninajua kuwa yuko hai kwa sababu anapepea bila upepo!)
Ombi kwa ajili ya Roho Mtakatifu
Ombeni pamoja kwa ajili ya Roho Mtakatifu. Daini ahadi ya Luka 11:13.
Chunguza Neno
Soma Luka 1:1-4 na Matendo ya Mitume 1:1-3. Kwa nini Luka aliandika injili ya Luka na kitabu cha Matendo ya Mitume?
Ni kwa namna gani maelezo ya Luka 24:36-43 ni kielelezo cha Matendo ya Mitume 1:3?
Hekima kutoka kwa Ellen White:
Kabla ya kupaa kwenda mbinguni, Kristo aliwapatia wanafunzi Wake agizo. Aliwaambia kuwa walitakiwa kuwa watekelezaji wa mapenzi Yake ambayo katika hayo alikuwa ameurithisha ulimwengu hazina za uzima wa milele. Aliwaambia wanafunzi Wake kuwa, mmekuwa mashahidi wa maisha yangu ya kujitoa kafara kwa niaba ya ulimwengu. Mmeziona kazi zangu nilizokuwa nafanya kwa ajili ya Israeli. Sasa ingawa watu wangu hawakuja kwangu ili wapate uzima, japo wakuu na makuhani amenifanyia mambo hayo kama walivyokuwa wamekusudia, ingawa wamenikataa, bado watakuwa na fursa nyingine ya kumpokea Mwana wa Mungu. Mmeona ya kwamba wote wanaonijia wakiungama dhambi zao ninawapokea bila masharti. Yeyote ajaye kwangu, sitamtupa nje kamwe. Kwenu wanafunzi Wangu, ninauweka ujumbe wa rehema. Unapaswa upelekwe kwa Wayahudi na Wamataifa – anzeni kwanza na Israeli, halafu mtakwenda mbele kwa mataifa yote, lugha na

jamaa. Wote watakaoamini imewapasa kuwakusanya katika kanisa moja. (Matendo ya Mitume, Sehemu ya Kwanza, uk. 21)
Kusudi la Ombi
Ombeni pamoja kwamba kila mtu katika familia na marafiki zenu amjue Yesu kama Mwokozi aliye hai. Baada ya kuombeana, omba kwa kutaja jina kwa ajili ya familia na marafiki ambao hawajamfahamu Yesu kwa namna binafsi iliyo hai.
Familia ya Kanisa
Utaratibu wa Mkusanyiko wa Jioni ya Kwanza
Katika usiku wa kwanza wa Siku 10 za Maombi, wahudhuriaji wawekwe katika vikundi vidogo vidogo vyenye vizazi mchanganyiko vya watu sita au pungufu. Kila kikundi kitaongozwa na mtu mzima mmoja na kijana mmoja, kama inavyoelezwa katika mwongozo wa kiongozi. Wahudhuriaji wanaweza kubakia katika vikundi hivyo kwa siku zote 10. (Ikiwa watu wapya watahudhuria katika usiku unaofuata, wasaidie kuunganishwa na kundi lililo tayari au kuunda kundi jipya ikiwa ni lazima.)
Kila usiku, wanaohudhuria wanaweza kukaaa kwa makundi yao huku kiongozi wa maombi anapotoa mwongozo wa maombi na shughuli akiwa mbele. Viongozi wa vikundi vidogo watarahisisha majadiliano ndani ya makundi yao pale wanapohimizwa. Wakati mwingine wahudhuriaji wote watashiriki pamoja, wakati mwingine wataomba na kujadili na wanakikundi wa kundi lao dogo na wakati mwingine watahimizwa kuomba kimya. Kiongozi wa maombi aliye na ustadi na mpana wa mawazo anaweza kwenda mbele zaidi kwa urahisi kati ya shughuli na kubadilisha maudhui kulingana na mahitaji ya eneo mahalia.

Ukaribisho
Ibada katika Maombi
KIONGOZI KWA WOTE: Kaeni katika vikundi vidogo. Timu yetu ya maombi itaalika kundi lako dogo kuomba pamoja kupitia Neno la Mungu. Baada ya kuomba kwa dakika chache, mtasikia timu ya maombi ikianza kuimba ubeti mmoja wa wimbo. Wakati huo, tafadhali hama kutoka kwenye maombi hadi kwenye wimbo.
Sifu:
(VIKUNDI VIDOGO) Katika Biblia zenu fungua Isaya 53, tafuteni sifa maalumu za Yesu. Mshukuruni Mungu kwa kila sifa ya Yesu.
(WOTE) Imbeni wimbo wa sifa.
Tubu:
(VIKUNDI VIDOGO) Soma Isaya 53:5. Tumia muda kwa ajili ya maombi binafsi ya ungamo la dhambi.
(WOTE) Imbeni wimbo wa neema ya Mungu.
Omba:
(VIKUNDI VIDOGO) Soma Yohana 16:13. Ombeni kwa ajili ya Roho Mtakatifu kuja na kutufundisha ukweli.
(WOTE) Imbeni wimbo wa Roho Mtakatifu.
Shughuli ya Kushirikiana
KIONGOZI KWA WOTE: Tengeneza vikundi vidogo vya watu wawili au watatu. Muulizane, “Ni vitu gani vitatu ungependa watu wajue kuhusu wewe?” Shiriki kwa dakika kadhaa. Sote tunayo mambo mengi ya kuvutia ambayo tunaweza kujifunza kuhusu kila mmoja. Baada ya Yesu kufa msalabani na kufufuka kutoka kaburini,

alikuwa na jambo maalumu ambalo alitaka kila mtu alijue kumhusu Yeye.
Ibada katika Neno
(VIKUNDI VIDOGO)
Soma Matendo ya Mitume 1:1-3. Tafadhali zingatia katika aya ya 3 kile ambacho Yesu alitaka kila mtu akifahamu. Yesu aliwadhihirishia “nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai.”
Soma Luka 24:13-32. Hususan zingatia aya ya 27. Yesu alifanya nini ili kujidhihirisha Yeye Mwenyewe kwa wanafunzi wawili?
Zingatia aya ya 32. Ushuhuda binafsi wa wanafunzi wale wawili baada ya kutambua kuwa walikuwa na Mwokozi aliye hai ulikuwaje?
Hekima kutoka kwa Ellen White:
Hivyo Kristo aliwaeleza wanafunzi Wake akizifungua akili zao ili wapate kuyaelewa Maandiko. Wanafunzi walikuwa wamechoka, lakini mazungumzo hayakuchosha. Maneno ya uzima na uthibitisho yalitoka katika midomo ya Mwokozi. Lakini bado macho yao yalikuwa yanamtazama. Alipokuwa akiwaambia juu ya kuangamizwa kwa Yerusalemu, waliutazama mji kwa huzuni. Lakini hata hivyo hawakuweza kukisia kwamba mtu wanayesafiri naye ni nani. Hawakufikiri kwamba mhusika wa mazungumzo yao alikuwa anatembea pamoja nao; maana Kristo alijizungumzia kana kwamba ni mtu mwingine. Walidhani kuwa alikuwa ni miongoni mwa wale ambao walihudhuria sikukuu kubwa na ambaye sasa alikuwa anarejea nyumbani kwake. Alitembea kwa uangalifu sana katika njia ya mawe kama wao, hapa na pale akisimama kupumzika kidogo. Hivyo ndivyo walisafiri katika

barabara ile ya milima milima, wakati Yule ambae muda mfupi ujao angekaa mkono wa kuume katika kiti cha enzi cha Mungu na ambaye angesema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani,” akitembea pembeni yao. Mathayo 26:18. (Tumaini la Vizazi Vyote, Sehemu ya Pili, uk. 410)
Kusudi la Ombi
KIONGOZI KWA WOTE: Wakati mwingine kama Wakristo, tunafanya kama vile Yesu Kristo bado yuko kaburini! Yesu alitumia siku 40 baada ya ufufuo Wake kuwathibitishia wafuasi Wake waaminifu kwamba Yeye ni Mwokozi ALIYE HAI.
Hebu tuombe katika vikundi vyetu kwamba hatutakuwa vipofu kwa Mwokozi wetu Aliye hai. Hebu tuombe kwamba Mungu angefungua macho yetu ili tujue kuwa Yesu yu hai na anajidhihirisha katika maisha yetu kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
Wito
KIONGOZI KWA WOTE: Ni nani hapa usiku huu anayeona haja ya kuutoa upya moyo wake kwa Mwokozi Aliye hai na kumjua Yeye zaidi kila siku? Ninawaalika wote wanaotaka kuitoa upya mioyo yao kwa Yesu kama Mwokozi Aliye hai, mpige magoti hapo mlipo.
Changamoto katika Saa 24
KIONGOZI KWA WOTE: Katika saa 24 zijazo, zima vifaa vyote vya kielektroniki kwa dakika 10. Soma Zaburi 46 peke yako—wewe na Mungu tu. Msifu Yesu Kristo kwa kuwa Mungu aliye hai! Mwombe Roho Mtakatifu amuweke mtu mmoja katika moyo wako na mshirikishe mtu huyo sababu moja unayoijua kwamba Yesu yu hai. Soma Matendo ya Mitume 1:6-8 kama maandalizi kwa ajili ya kesho.

+ Show More
– Show Less